NIJUAVYO MIMI Read Count : 35

Category : Articles

Sub Category : Spirituality
Kwamba:

- Kazi ya mdomo ni kulisha tumbo; bali kazi ya ulimi ni kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa kumwimbia tenzi na zaburi.

- Kazi ya macho ni kumwepuka adui na kutafuta mahali salama pa kujihifadhi.

- Kazi ya mikono ni kutafuta riziki kwa kufanya kazi  halali na ya haki kwa bidii zote. 

- Kazi ya miguu ni kumwahisha mwanadamu mahali pa ibada kwanza;  kisha mahali pa kupatia riziki na hatimaye  kumrejesha mahali pake pa kujihifadhi panapoitwa nyumbani.

- Lakini kazi ya 'moyo' na 'nafsi' ni kumsimamia huyu mtu kuwa kiumbe chenye uhai endelevu amchaye Mwenyezi Mungu na kuendeleza maisha yake hapa duniani kwa ufanisi. 

Hatuwezi kuendelea kuitwa Wanadamu endapo maisha yetu yanakinzana na ukweli huo hapo juu japo kwa uchache.

Ikiwa mdomo haufanyi kazi ya kulisha mwili chakula bora kwa afya ya mwili, faida yake ni nini?

Haiwezekani pombe, sigara, bangi, vyakula vinavyo haribu afya na sumu vikaingizwa mwilini na mwili usidhurike.

Afya yako ni tafsiri rahisi ya nini kiingiacho mwilini mwako au kutokuingia. Tutasoma alama za ulafi na kukosa kiasi au ukosefu wa lishe ya kutosha na bora kwa kuutazama mwili wako ulivyo. Muonekano huo ni alama ya kukosa ufahamu juu ya namna ya kutambua mpango mahsusi wa ulaji na aina ya vyakula vya kula kwa wale ambao kwao chakula si tatizo. Jifunze kanuni za lishe bora. 

Ulimi wako usiwe moto bali baridi. Ulimi wako usiwe lango la uharibifu bali chemchem ya amani, sifa na utukufu kwa Mungu. Usiuachie ulimi wako kuwa kisu cha kuwakata wengine bali mlango wa amani na upatanisho. Acha ulimi wako daima uwe bubujiko la ibada kwa Mungu Baba wa Mbinguni.

Mwimbie Mungu tenzi na zaburi milele.  

Kwa ulimi wako  jishibishe amani, utulivu wa moyo na nafsi daima. 

Heri mtu yule aufungae ulimi wake lijamu na kuufanya mzito kwa mizaha na maneno yauchafuayo moyo na kuitia kiza nafsi yake na jirani yake!

Jicho ni kazi ya ajabu ya Mungu. Mimi hutafakari maajabu ya kuona hata nisipate hisia yoyote ya ufahamu. Sipati fununu hata za jinsi jicho liwezavyo kutenda kazi zake. Sifa, nguvu na utukufu vikuendee wewe Mungu milele.

Je, Mungu hakunitia macho ili nipate kuziona kazi zake na kutambua ukuu wake? 

Hakika ninaona; je, naona kwa nguvu, ukuu, sifa na utukufu wake Mungu au kwa uharibifu wangu mwenyewe?

Naijua kweli; nayo ndiyo hii: kwa macho yangu mawili natenda dhambi zaidi. Naona kwa hasara yangu na si kwa faida yangu ya sasa na ya maisha yadumuyo milele. Macho yangu ni 'banzi na boriti' kwangu! Mungu wangu, niumbie moyo na nafsi zenye nguvu za kuushinda na kuudhibiti udhaifu wa ndani unaotoka hadi nje!

Mungu, sitaki nikose kukaa pamoja na Yesu, Malaika, Mitume 12; tena, nimwone Adamu, Bibi yetu Eva na Lazaro shahidi aliyefufuliwa na Yesu na Watakatifu wengi. Nipe nguvu na uwezo wa kuyadhibiti macho.   Nataka nitatazame na kuona kila kitu mbele yangu  'kitakatifu' na si 'kiovu!' Amina!

Ee Mungu, mikono ni lango la baraka; nawe ulizibariki kazi za mikono ya mwanadamu. Mara kadhaa adui ameichafua mikono ya mwanadamu kupitia nguvu na uweza wa kihalifu katika ulimwengu wa maroho mabaya. Lakini Baba ni bayana na hakika ya kuwa kamwe  'giza' halijapata kuishinda 'nuru'. Tena NURU ndiye KRISTO mwenyewe. 

Baba, naichovya mikono yangu saa hii ndani ya DAMU YA YESU; naitakasa mikono hii kwa Damu hii takatifu na kuiamuru kuwa safi tena. Naamuru baraka za asili sawa sawa na kusudio la Mungu wakati wa uumbaji, kurejea mahali pake mara hii na kuwa baraka. Narejesha chochote kilichoibiwa mara dufu na kukitakasa kwa Damu ya Yesu. Natamka wewe uliyeibiwa na umerejea mara hii mara dufu, nakuamuru kuwa baraka kwa sifa na utukufu wake Mungu Yehova. 

Mikono yangu nakufunika kwa Damu ya Yesu. Mikono ya wana familia yangu naifunika kwa Damu ya Yesu. Kabarikiwe asubuhi; kabarikiwe mchana; kabarikiwe jioni; kabarikiwe na usiku. Amina.

Ewe mikono yangu, Kaskazini ikakushushie baraka za Abraham, Isaka na Yakobo. Ewe mikono yangu, Kusini ikakushushie baraka za Abraham, Isaka na Yakobo. Ewe mikono yangu, Magharibi isikupungukie kamwe, ikafikishe taarifa zako kwa Mamajusi wa Mashariki wakakufungashie sehemu ya hazina zao na kukuletea mapema ili utoke Tarshish na kwenda Ninawi yako sawa sawa na agizo la Mungu katika maisha yako.

Ewe mikono yangu, Mashariki haitanyamaza kwa ajili yako. Tazama ewe mikono yangu, Mashariki imeshikilia hazina zako walizozificha adui zako, piga kelele sasa useme:
"Ewe Mashariki, Bwana amenifunulia siri za uchawi wako na wizi wa nyota na hazina zangu; kama ' NIKO AMBAYE NIKO' aishivyo milele;
nakuamuru kuachia nyota na hazina zangu sasa katika Jina  la Yesu. Tena, nakuapiza kwa Jina la Yesu, usiinuke kamwe kurejea hazina hii au kujiinua vinginevyo juu yangu na familia yangu milele na milele yote katika Jina la Yesu na nguvu ya Damu ya Yesu. Amina!

Ewe mikono yangu, nakutamkia kuanzia sasa ya kuwa wewe ni baraka. Ndani yako zimo baraka za Abraham, Isaka na Yakobo; lakini pia zimo hazina za Mashariki. Chochote utakachoshika kitakuwa dhahabu safi na yenye thamani kubwa itakayogombewa na wachuuzi wa pande zote za dunia. Tazama, wewe ni lulu aghali sana. Tazama, wewe ni fedha ya kigeni yenye thamani kubwa. Tazama, katika michoro ya viganja vyako, humo yameandikwa majina ya vito vyote vyenye thamani kubwa wavipendavyo Wafalme na Malkia wao. Yamo majina ya nyota zote kuu zenye nguvu ya utajiri, umiliki, utawala, hekima, akili, maarifa na heshima. Inuka sasa ee mikono yangu ukafanye kazi ili ule haki yako iliyomo ndani yako mwenyewe. Kaguse ardhi, ifumuke dhahabu, yakuti, marijani, samawati na chakula kingi na kitamu kama mana.

Ee mikono yangu, nenda sasa kafurahie uumbaji wa Mungu wako wa Mbinguni tena usimsahau kwa matoleo yako yaliyo safi na stahiki machoni pake ili daima aachilie Malaika zake kukutembelea na kukushushia mvua  au umande wa Mbinguni kwa majira yake. Amina!

Ewe miguu yangu, ijapo wewe ni mtii, usiyegoma kwa dharau au kiburi, nimekulazimisha kwenda huku na huko kwa hasara yangu. Sasa nisamehe na tuweke ushirika baina yangu mimi na wewe. Kwamba, kuanzia sasa, sisi ni watumishi wa Bwana. Moyo, nafsi na miguu tunaungana kumtumikia Mungu.  
Popote miguu hii itakapokwenda itakuwa ni kwa utukufu wake YEHOVA.
Ee Mungu nipe nguvu na uwezo wa kutimiza ahadi hii kwa uaminifu. Tena nitendapo haya kwa uaminifu, ee Mungu, unibariki na kuniwekea Malaika wa kunilinda mimi na familia yangu daima. Amina!


Abraham Blessings

255789175797

Comments

  • One of the best online tool for writers. It's our WRITINGS BANK acting as a safe place for storage yet a platform for global communications.

    Aug 23, 2020

Log Out?

Are you sure you want to log out?